6 Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng’ombe walikunguwaa.
7 Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu.
8 Daudi akaona uchungu kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo.
9 Naye Daudi akamwogopa BWANA siku ile; akasema, Litanijiaje sanduku la BWANA?
10 Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la BWANA kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti.
11 Sanduku la BWANA akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote.
12 Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, BWANA ameibarikia nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe.