3 nami nitamkatilia mbali mwamuzi atoke kati yake, nami nitawaua wakuu wake pamoja naye, asema BWANA.
4 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA; wala hawakuzishika amri zake; na maneno yao ya uongo yamewakosesha, ambayo baba zao waliyafuata;
5 lakini nitapeleka moto juu ya Yuda, nao utayateketeza majumba ya Yerusalemu.
6 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu;
7 nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya mwenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu;
8 nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha.
9 Lakini nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini.