1 Lisikieni neno hili, enyi ng’ombe wa Bashani, mnaokaa juu ya mlima wa Samaria, mnaowaonea maskini, na kuwaponda wahitaji; mnaowaambia bwana zao, Haya! Leteni, tunywe.
2 Bwana MUNGU ameapa kwa utakatifu wake, ya kuwa, tazama, siku zitawajilia, watakapowaondoa ninyi kwa kulabu, na mabaki yenu kwa ndoana.
3 Nanyi mtatoka kwenye mahali palipobomolewa, kila mwanamke moja kwa moja mbele yake; nanyi mtajitupa katika Harmoni, asema BWANA.
4 Njoni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu;
5 mkachome sadaka ya shukrani, ya kitu kilichotiwa chachu; mkatangaze sadaka mtoazo kwa hiari na kuzihubiri habari zake; kwa maana ndivyo viwapendezavyo ninyi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana MUNGU.