1 Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, kikapu cha matunda ya wakati wa hari.
2 Akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona kikapu cha matunda ya wakati wa hari. Ndipo BWANA akaniambia, Mwisho wao umewajilia watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe.
3 Tena nyimbo za hekaluni zitakuwa vilio siku ile, asema Bwana MUNGU; mizoga itakuwa mingi; kila mahali wataitupa, wakinyamaza kimya.
4 Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi,
5 mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu;
6 tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano.