1 Nalimwona Bwana akisimama karibu na madhabahu; akasema, vipigo vichwa vya nguzo, hata vizingiti vitikisike; vivunje vipande vipande juu ya kichwa cha kila mmoja wao; nami nitamwua mtu wa mwisho wao kwa upanga; hapana hata mmoja wao atakayekimbia, wala hataokoka hata mmoja wao.
2 Wajapochimba waingie katika kuzimu, mkono wangu utawatoa huko; nao wajapopanda hata mbinguni, nitawatelemsha toka huko.
3 Nao wajapojificha katika kilele cha Karmeli, nitawatafuta na kuwatoa toka huko; na wajapositirika katika vilindi vya bahari nisiwaone, nitamwagiza joka huko, naye atawauma.
4 Nao wajapokwenda hali ya kufungwa mbele ya adui zao, nitauagiza upanga huko, nao utawaua; nami nitawaelekezea macho yangu niwatende mabaya, wala si mema.