1 Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza BWANA, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao?
2 BWANA akasema, Yuda atakwea; tazama, nimeitia hiyo nchi mkononi mwake.
3 Ndipo Yuda akamwambia Simeoni ndugu yake, Kwea wewe pamoja nami katika kura yangu, ili tupate kupigana na Wakanaani; kisha mimi nami nitakwenda pamoja nawe katika kura yako. Basi Simeoni akaenda pamoja naye.
4 Yuda akakwea; naye BWANA akawatia Wakanaani na Waperizi mkononi mwao; nao wakawapiga huko Bezeki watu elfu kumi.
5 Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi.
6 Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya miguu.
7 Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko.