10 Ndipo wana wa Israeli wakamlilia BWANA, wakisema, Sisi tumekufanyia dhambi, kwa sababu tumemwacha Mungu wetu, na kuyatumikia Mabaali.
11 Naye BWANA akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti?
12 Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao.
13 Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena.
14 Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu.
15 Wana wa Israeli wakamwambia BWANA Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu.
16 Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia BWANA; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli.