6 Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi.
7 Watu hao wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya BWANA yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
8 Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi.
9 Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.
10 Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
11 Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali.
12 Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika.