3 aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi.
4 Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za BWANA, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa.
5 Basi wana wa Israeli wakaketi kati ya Wakanaani; hao Wahiti, na hao Waamori, na hao Waperizi, na hao Wahivi na hao Wayebusi;
6 wakawaoa binti zao, na binti zao wenyewe wakawaoza wana wao waume, na kuitumikia miungu yao.
7 Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakamsahau BWANA, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi.
8 Kwa hiyo hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane.
9 Kisha wana wa Israeli walipomlingana BWANA, BWANA akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.