11 Malaika wa BWANA akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani.
12 Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa.
13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani.
14 BWANA akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma?
15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.
16 BWANA akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.
17 Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami.