1 Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Shekemu kwa ndugu za mama yake, akanena nao, na wote waliokuwa wa nyumba ya baba ya mama yake, akasema,
2 Haya, neneni tafadhali masikioni mwa waume wote wa Shekemu, mkaulize, Je! Ni lipi lililo jema kwenu, kwamba hao wana wa Yerubaali wote, ambao ni watu sabini, watawale juu yenu, au kwamba mtu mmoja atawale juu yenu? Tena kumbukeni ya kwamba mimi ni mfupa na nyama yenu.
3 Hao ndugu za mama yake wakanena habari zake masikioni mwa hao watu wote wa Shekemu maneno hayo yote; na mioyo yao ikaelekea kumwandama Abimeleki; kwa kuwa walisema, Huyu ni ndugu yetu.
4 Wakampa vipande vya fedha sabini vilivyotoka katika nyumba ya Baal-berithi, na kwa fedha hizo Abimeleki akaajiri watu wapuuzi mabaradhuli, wafuatane naye.
5 Kisha akaenda nyumbani kwa babaye huko Ofra, akawaua nduguze, hao wana wa Yerubaali, watu sabini, akawaua juu ya jiwe moja; lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubaali, alisalia; kwa maana alijificha.
6 Kisha hao watu wote wa Shekemu wakakusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu.