16 Basi sasa ikiwa mmetenda kwa uaminifu na uelekevu, katika kumtawaza Abimeleki awe mfalme, na ikiwa mmemtendea mema Yerubaali na nyumba yake, na kumtendea kama ilivyostahili mikono yake;
17 (kwa maana baba yangu aliwatetea ninyi, na kuhatirisha uhai wake, na kuwaokoa na mikono ya Midiani;
18 nanyi mmeinuka juu ya nyumba ya baba yangu hivi leo nanyi mmewaua wanawe, watu sabini, juu ya jiwe moja, nanyi mmemtawaza Abimeleki, mwana wa kijakazi chake, awe mfalme juu ya watu wa Shekemu kwa sababu yeye ni ndugu yenu;)
19 basi ikiwa mmemtendea kwa uaminifu na uelekevu Yerubaali na nyumba yake hivi leo, basi furahini ninyi katika huyo Abimeleki, yeye naye na afurahi kwenu ninyi;
20 lakini kwamba sivyo hivyo, basi, moto na utoke katika Abimeleki na kuwateketeza watu wa Shekemu, na jamaa ya Milo; kisha moto na utoke katika hao watu wa Shekemu, na katika jamaa ya Milo, na kumteketeza Abimeleki.
21 Kisha Yothamu akaenda zake na kukimbia, akaenda Beeri, na kukaa kuko, kwa kumwogopa Abimeleki nduguye.
22 Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu.