11 Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria,
12 Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe.
13 Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona.
14 Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi.
15 Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme.
16 Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu.
17 Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto.