3 Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;
4 vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.
5 Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
6 Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria.
7 Mkuu wa matowashi akawapa majina; alimwita Danieli, Belteshaza; na Hanania akamwita Shadraka; na Mishaeli akamwita Meshaki; na Azaria akamwita Abednego.
8 Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi.
9 Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi.