10 wala hatukuitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.
11 Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi.
12 Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu.
13 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake.
14 Basi BWANA ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana BWANA, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake.
15 Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu.
16 Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka.