1 Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu.
2 Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini,
3 neno la BWANA lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa BWANA ulikuwa hapo juu yake.
4 Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo.
5 Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu.
6 Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne.
7 Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana.