17 Waliposimama hao, hayo nayo yalisimama; na walipopaa juu hao, hayo nayo yalipaa juu pamoja nao; maana roho ya huyo kiumbe hai ilikuwa ndani yao.
18 Kisha huo utukufu wa BWANA ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya makerubi.
19 Nao makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu, hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya BWANA; na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.
20 Huyu ndiye kiumbe hai niliyemwona, chini ya Mungu wa Israeli, karibu na mto Kebari; nikajua ya kuwa hao ni makerubi.
21 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne; na mifano ya mikono ya mwanadamu ilikuwa chini ya mabawa yao.
22 Na mfano wa nyuso zao, ni nyuso zile zile nilizoziona karibu na mto Kebari; kuonekana kwao, na wao wenyewe; kila mmoja walikwenda mbele moja kwa moja.