1 Tena roho ikaniinua, ikanileta hata lango la upande wa mashariki wa nyumba ya BWANA, lililoelekea upande wa mashariki; na tazama, mahali pa kuingilia pa lango walikuwako watu ishirini na watano; na katikati yao nikamwona Yaazania, mwana wa Azuri, na Pelatia, mwana wa Benaya, nao ni wakuu wa watu.
2 Akaniambia, Mwanadamu, hawa ndio watu wale watungao uovu, na kutoa mashauri mabaya ndani ya mji huu;
3 wasemao, Wakati wa kujenga nyumba si karibu; mji huu ni sufuria na sisi ni nyama.
4 Basi toa unabii juu yao, Ee mwanadamu, toa unabii.
5 Roho ya BWANA ikaniangukia, naye akaniambia, Nena, BWANA asema hivi; Mmesema maneno hayo, Enyi nyumba ya Israeli; maana mimi nayajua yaingiayo katika mioyo yenu.
6 Mmewaongeza watu wenu waliouawa ndani ya mji wenu, nanyi mmezijaza njia kuu zake waliouawa.
7 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Watu wenu waliouawa, ambao mmewalaza katikati yake, hao ndio nyama hiyo, na mji huu ndio sufuria; lakini ninyi mtatolewa nje kutoka katikati yake.