42 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu.
43 Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda.
44 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si sawasawa na njia zenu mbaya, wala si sawasawa na matendo yenu mabovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU.
45 Neno la BWANA likanijia, kusema,
46 Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu,
47 ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hata kaskazini zitateketezwa kwa moto huo.
48 Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, BWANA, nimeuwasha; hautazimika.