14 Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote.
15 Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje.
16 Jiweke tayari, enenda upande wa kuume; jipange, enenda upande wa kushoto; mahali po pote utakapouelekeza uso wako.
17 Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili.
18 Neno la BWANA likanijia tena, kusema,
19 Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini.
20 Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma.