18 Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.
19 Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.
20 Neno la BWANA likanijia, kusema,
21 Mwanadamu, uuelekezee Sidoni uso wako, ukatabiri juu yake,
22 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Sidoni, nami natukuzwa kati yako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu ndani yake, na kutakasika ndani yake.
23 Maana nitampelekea tauni, na damu, katika njia kuu zake, na hao waliotiwa jeraha wataanguka kati yake, kwa upanga juu yake pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
24 Wala hautakuwapo mchongoma uchomao kwa nyumba ya Israeli; wala mwiba uumizao miongoni mwa wote wamzungukao, waliowatenda mambo ya jeuri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.