18 Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
19 Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.
20 Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
21 Bali ukimwonya mwenye haki, kwamba yule mwenye haki asitende dhambi, tena ikiwa yeye hatendi dhambi, hakika ataishi, kwa sababu alikubali kuonywa; nawe umejiokoa roho yako.
22 Na mkono wa BWANA ulikuwako juu yangu huko; akaniambia, Ondoka, enenda uwandani; nami nitasema nawe huko.
23 Basi, nikaondoka, nikaenda uwandani, na tazama, utukufu wa BWANA ulisimama huko, kama utukufu ule niliouona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.
24 Ndipo roho ile ikaniingia, ikanisimamisha kwa miguu yangu; akasema nami, akaniambia, Enenda ukajifungie nyumbani mwako.