10 Nami nitawashangaza watu wa kabila nyingi kwa habari zako, na wafalme wao wataogopa sana kwa ajili yako, nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao; nao watatetemeka kila dakika, kila mtu kwa ajili ya uhai wake, katika siku ya kuanguka kwako.
11 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Upanga wa mfalme wa Babeli utakujilia.
12 Kwa panga za mashujaa nitawaangusha watu wako wote jamii; hao wote ni watu wa mataifa watishao, nao watakiharibu kiburi cha Misri, na jamii ya watu wake wengi wataangamia.
13 Tena nitawaharibu wanyama wake wote, toka kando ya maji mengi; na mguu wa mwanadamu hautayatibua tena, wala kwato za mnyama hazitayatibua.
14 Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU.
15 Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
16 Hayo ndiyo maombolezo watakayoomboleza; binti za mataifa wataomboleza kwa hayo; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.