Eze. 46:8-14 SUV

8 Naye mkuu atakapoingia, ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango lile, naye atatoka kwa njia iyo hiyo.

9 Lakini watu wa nchi watakapokuja mbele za BWANA katika sikukuu zilizoamriwa, yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kaskazini ili kuabudu, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kusini; na yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kusini, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kaskazini; hatarudi kwa njia ya lango aliloingia kwalo, lakini atatoka kwa kwenda mbele moja kwa moja.

10 Naye mkuu atakapoingia, ataingia katikati yao, nao, watakapotoka, watatoka wote pamoja.

11 Na katika sikukuu hizo, na sikukuu nyingine zilizoamriwa, sadaka ya unga itakuwa efa moja kwa ng’ombe mmoja, na efa moja kwa kondoo mume mmoja, na kwa wale wana-kondoo kiasi awezacho kutoa, na hini moja ya mafuta kwa efa moja.

12 Naye mkuu atakapotengeneza sadaka atoayo kwa hiari yake mwenyewe, sadaka ya kuteketezwa, au sadaka za amani, ziwe sadaka amtoleazo BWANA kwa hiari yake mwenyewe, mtu mmoja atamfungulia lango lile lielekealo upande wa mashariki, naye ataitengeneza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka zake za amani, kama afanyavyo siku ya sabato; kisha atatoka; na baada ya kutoka kwake mtu mmoja atalifunga lango.

13 Nawe utatengeneza mwana-kondoo wa mwaka wa kwanza, mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA kila siku; kila siku asubuhi utamtengeneza.

14 Nawe utatengeneza sadaka ya unga pamoja nayo kila siku asubuhi, sehemu ya sita ya efa moja, na sehemu ya tatu ya hini moja ya mafuta; kuchanganya na unga ule mzuri; sadaka ya unga kwa BWANA daima, kwa amri ya milele.