5 Nami nitaiweka mizoga ya wana wa Israeli mbele ya vinyago vyao; nami nitaitawanya mifupa yenu pande zote za madhabahu zenu.
6 Kila mahali mkaapo miji itaharibika, na mahali palipoinuka patakuwa ukiwa; ili madhabahu zenu ziharibiwe, na kufanywa ukiwa, na vinyago vyenu vivunjwe, na kukoma, na sanamu zenu za jua zikatwe, na kuangushwa, na kazi zenu zifutwe kabisa.
7 Na hao waliouawa wataanguka katikati yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
8 Lakini nitasaza mabaki; maana mtakuwa na baadhi ya watu watakaoukimbia upanga kati ya mataifa, mtakapokuwa mmetawanyika katika nchi za watu.
9 Na hao wa kwenu watakaookoka watanikumbuka kati ya mataifa, watakakochukuliwa mateka, jinsi nilivyoiponda mioyo yao ya kikahaba, iliyoniacha, na macho yao, yaendayo kufanya uasherati na vinyago vyao; nao watajichukia nafsi zao machoni pao wenyewe, kwa sababu ya mabaya yao yote, waliyoyatenda kwa machukizo yao yote.
10 Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; sikusema bure kama nitawatenda mabaya hayo.
11 Bwana MUNGU asema hivi; Piga kwa mkono wako, ipige nchi kwa mguu wako, ukaseme, Ole! Kwa sababu ya machukizo maovu yote ya nyumba ya Israeli; maana wataanguka kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.