1 Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, hekalu,
2 wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa mbari za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi twamtolea dhabihu tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa.
3 Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa mbari za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru.
4 Ndipo watu wa nchi wakaidhoofisha mikono ya watu wa Yuda, wakawasumbua, walipokuwa wakijenga.
5 Wakawaajiri washauri juu yao, ili kuwapinga kusudi lao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.
6 Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu.
7 Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na mabaki ya wenziwe, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kunenwa kwa lugha ya Kiaramu.