Ezr. 6:8-14 SUV

8 Tena, natoa amri kuwaagiza ninyi mtakayowatendea wazee hao wa Wayahudi, kwa kazi hii ya kuijenga nyumba ya Mungu; katika mali ya mfalme, yaani, katika kodi za nchi iliyo ng’ambo ya Mto, watu hao wapewe gharama zote kwa bidii, ili wasizuiliwe.

9 Na kila kitu wanachokihitaji, katika ng’ombe wachanga, na kondoo waume, na wana-kondoo, kwa sadaka za kuteketezwa watakazomtolea Mungu wa mbinguni, na ngano, na chumvi, na divai, na mafuta, kama makuhani walioko Yerusalemu watakavyosema, na wapewe vitu hivyo vyote siku kwa siku, msikose kuwapa;

10 wapate kumtolea Mungu wa mbinguni sadaka zenye harufu nzuri, na kumwombea mfalme, na wanawe, wapate uzima.

11 Pia nimetoa amri kwamba, mtu awaye yote atakayelibadili neno hili, boriti na itolewe katika nyumba yake, akainuliwe na kutungikwa juu yake; tena nyumba yake ikafanywe jaa kwa ajili ya neno hili.

12 Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na watu wote, watakaonyosha mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na ifanyike kwa bidii nyingi.

13 Ndipo Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzi wao, wakafanya hayo kwa bidii, kwa sababu mfalme Dario alikuwa ametuma watu kwao.

14 Nao wazee wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa, kwa msaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido. Wakajenga, wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi.