16 Kisha BWANA akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe.
17 Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako.
18 Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa BWANA, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo BWANA atawapa nyama, nanyi mtakula.
19 Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini;
20 lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa BWANA aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani?
21 Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima.
22 Je! Makundi ya kondoo na ng’ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha?