1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na Haruni, ukamwambie, Utakapoziweka taa, hizo taa saba zitatoa nuru hapo mbele ya kinara cha taa.
3 Basi Haruni akafanya; akaziweka taa zake ili zitoe nuru hapo mbele ya kinara, kama BWANA alivyomwagiza Musa.
4 Na hii ndiyo kazi ya hicho kinara cha taa, ilikuwa ni kazi ya ufuzi wa dhahabu; tangu tako lake hata maua yake kilikuwa ni kazi ya ufuzi; vile vile kama ule mfano BWANA aliokuwa amemwonyesha Musa, ndivyo alivyokifanya kinara.
5 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
6 Watwae Walawi na kuwaondoa kati ya wana wa Israeli, kisha uwatakase.
7 Nawe utawafanyia mambo haya ili kuwatakasa; nyunyiza juu yao maji yatakasayo dhambi, nao wajinyoe kwa wembe mwili wote, kisha wazifue nguo zao, na kujitakasa.
8 Kisha na watwae ng’ombe mume mmoja mchanga, na sadaka yake ya unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, nawe utatwaa ng’ombe mume mchanga mwingine kuwa sadaka ya dhambi.
9 Nawe utawahudhurisha Walawi mbele ya hema ya kukutania; nawe utaukutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli;
10 nawe utawahudhurisha Walawi mbele za BWANA; kisha wana wa Israeli wataweka mikono yao juu ya Walawi;
11 naye Haruni atawasongeza Walawi mbele za BWANA wawe sadaka ya kutikiswa, kwa ajili ya wana wa Israeli, ili wawe wenye kufanya utumishi wa BWANA.
12 Kisha Walawi wataweka mikono yao juu ya vichwa vya hao ng’ombe; nawe umtoe mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa BWANA, na huyo wa pili awe sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.
13 Kisha utawaweka Walawi mbele ya Haruni, na mbele ya wanawe na kuwasongeza kwa BWANA wawe sadaka ya kutikiswa.
14 Ndivyo utakavyowatenga Walawi na kuwatoa katika wana wa Israeli; na Walawi watakuwa wangu.
15 Kisha baadaye Walawi wataingia ndani, ili wafanye utumishi wa hema ya kukutania; nawe utawatakasa, na kuwasongeza wawe sadaka ya kutikiswa.
16 Kwa kuwa nimepewa kabisa mimi watu hawa kutoka katika wana wa Israeli; badala ya wote wafunguao mimba, maana, wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli wote, nimewatwaa wawe wangu.
17 Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli ni wangu, wa wanadamu na wa wanyama; siku hiyo niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri niliwatakasa kwa ajili yangu mwenyewe.
18 Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote walio katika wana wa Israeli.
19 Nami nimempa Haruni hao Walawi wawe kipawa chake yeye na wanawe, kutoka kwa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa wana wa Israeli katika hema ya kukutania, kisha wafanye upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli; ili kusiwe na maradhi kati ya wana wa Israeli, hapo wana wa Israeli watakapopakaribia mahali patakatifu.
20 Basi Musa na Haruni, na mkutano wote wa wana wa Israeli, wakawafanyia Walawi mambo hayo; kama hayo yote BWANA aliyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo wana wa Israeli walivyowafanyia.
21 Walawi wakajitakasa na dhambi, nao wakafua nguo zao; kisha Haruni akawasongeza mbele za BWANA wawe sadaka ya kutikiswa; Haruni akafanya kwa ajili yao ili kuwatakasa.
22 Kisha baada ya hayo Walawi wakaingia ili wafanye utumishi wao ndani ya hema ya kukutania mbele ya Haruni na mbele ya wanawe; kama BWANA alivyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo walivyowafanyia.
23 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
24 Mambo yawapasayo hao Walawi ni haya; tangu waliopata umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi wataingia ndani ili watumike utumishi katika kazi ya hema ya kukutania;
25 tena tangu waliopata umri wa miaka hamsini wataacha kutumika huo utumishi, wasitumike tena;
26 lakini watatumika pamoja na ndugu zao katika hema ya kukutania, kushika ulinzi, lakini wasitumike katika huo utumishi tena. Ndivyo utakavyowafanyia Walawi katika mambo ya ulinzi wao.