1 Wakati huo wakakaribia hao binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
2 Nao wakasimama mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema,
3 Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha BWANA katika mkutano wa Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume.
4 Kwa nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu.
5 Basi Musa akaleta neno lao mbele ya BWANA
6 BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
7 Hao binti za Selofehadi wananena lililo haki; kweli utawapa milki ya urithi pamoja na ndugu za baba yao; nawe utawapa urithi wa baba yao.
8 Kisha utanena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtu akifa, naye hana mwana wa kiume, ndipo utampa binti yake urithi wake.
9 Tena ikiwa hana binti, mtawapa nduguze urithi wake.
10 Na ikiwa hana ndugu, mtawapa ndugu za babaye huo urithi wake.
11 Tena ikiwa babaye hana ndugu, utampa huyo aliye karibu naye katika jamaa zake huo urithi wake, naye atakuwa nao; na neno hili litakuwa ni amri ya hukumu kwa wana wa Israeli, kama BWANA alivyomwagiza Musa.
12 BWANA akamwambia Musa, Panda wewe juu ya mlima huu wa Abarimu, uitazame nchi niliyowapa wana wa Israeli.
13 Na ukiisha kuiona, wewe nawe utakusanyika pamoja na baba zako, kama Haruni ndugu yako alivyokusanyika;
14 kwa sababu mliasi juu ya neno langu katika jangwa la Sini wakati wa mateto ya mkutano, wala hamkunistahi, hapo majini, mbele ya macho yao. (Maji hayo ndiyo maji ya Meriba ya Kadeshi katika jangwa la Sini.)
15 Musa akanena na BWANA akisema,
16 BWANA, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano,
17 atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa BWANA wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.
18 BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako;
19 kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao.
20 Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii.
21 Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia.
22 Musa akafanya kama BWANA alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote;
23 kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama BWANA alivyosema kwa mkono wa Musa.