8 Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi;
9 Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia;
10 tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia?
11 Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha BWANA; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung’unikia?
12 Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi;
13 je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa?
14 Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji.