1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;
2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.
3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za BWANA zikawaka juu ya Israeli.
4 Kisha BWANA akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie BWANA watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za BWANA ziwaondokee Israeli.
5 Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori.
6 Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania.