1 Kisha BWANA akanena na Musa katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko, akamwambia,
2 Uwaagize wana wa Israeli wawape Walawi miji wapate mahali pa kukaa, katika milki yao; pamoja na malisho yaliyoizunguka hiyo miji kotekote mtawapa Walawi.
3 Hiyo miji watakuwa nayo ili wakae humo, na malisho watakuwa nayo kwa wanyama wao wa mifugo, na kwa mali zao, na kwa wanyama wao wote.
4 Na yale malisho ya miji mtakayowapa Walawi, ukubwa wake utakuwa tangu ukuta wa mji kupima kiasi cha dhiraa elfu pande zote.