1 Israeli ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri.
2 Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao.
3 Yakini sasa watasema, Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi BWANA; na mfalme huyu je! Aweza kututendea nini?
4 Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba.
5 Wakaao Samaria wataona hofu kwa ajili ya ndama za Beth-Aveni; kwa maana watu wa mji huo wataulilia, na makuhani wake walioufurahia, kwa sababu ya utukufu wake; kwa maana umetoweka.