8 Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, Tuangukieni.
9 Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea; huko ndiko walikosimama; ili vita vilivyokuwa juu ya wana wa uovu visiwapate katika Gibea.
10 Wakati nitakapopenda nitawaadhibu; na hao mataifa watakusanyika juu yao, watakapofungwa kwa sababu ya makosa yao mawili.
11 Naye Efraimu ni ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; lakini nimepitisha kongwa juu ya shingo yake nzuri; nitampandisha mwenye kupanda juu ya Efraimu; Yuda atalima, na Yakobo atavunja madongoa yake.
12 Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta BWANA, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki.
13 Mmelima dhuluma, mmevuna uovu; mmekula matunda ya uongo; kwa maana uliitumainia njia yako, na wingi wa mashujaa wako.
14 Kwa sababu hiyo fitina itatokea kati ya watu wako, na ngome zako zote zitaharibiwa, kama vile Shalmani alivyoharibu Betharbeli, katika siku ya vita; mama akavunjika-vunjika pamoja na watoto wake.