14 Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele
15 Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba; siku hiyo ya kwanza mtaondoa chachu yote isiwe katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula mkate uliochachwa tangu siku hiyo ya kwanza hata siku ya saba, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na Israeli.
16 Siku ya kwanza kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa kazi yo yote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.
17 Nanyi mtaitunza ile sikukuu ya mikate isiyochachwa; kwa kuwa katika siku iyo hiyo mimi nimeyatoa majeshi yenu katika nchi ya Misri; kwa hiyo mtaitunza siku hiyo katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.
18 Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni.
19 Muda wa siku saba isionekane chachu katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula hiyo iliyotiwa chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa hali ya ugeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi.
20 Msile kitu chochote kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote.