5 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.
6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.
7 Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla.
8 Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu.
9 Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani.
10 Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto.
11 Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA.