1 Mtu akiiba ng’ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng’ombe watano badala ya ng’ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.
2 Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake.
3 Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake.
4 Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng’ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili.