29 Na Haruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele ya BWANA daima.
30 Nawe utie hizo Urimu na Thumimu katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu; nazo zitakuwa juu ya moyo wa Haruni, hapo atakapoingia ndani mbele ya BWANA; na Haruni atachukua hukumu ya hao wana wa Israeli juu ya moyo wake mbele ya BWANA daima.
31 Nawe fanya hiyo joho ya naivera ya rangi ya samawi yote.
32 Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke.
33 Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote;
34 njuga ya dhahabu na komamanga, njuga ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote.
35 Nayo itakuwa juu ya Haruni akitumika; na sauti ya hizo njuga itasikilikana hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya BWANA na hapo atokapo nje, ili kwamba asife.