23 utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya BWANA;
24 nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisa-tikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA.
25 Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele ya BWANA; ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
26 Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisa-tikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; nacho kitakuwa ni sehemu yako.
27 Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Haruni, na huyo aliyekuwa kwa ajili ya wanawe;
28 navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya BWANA.
29 Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu.