1 Kisha BWANA akamwambia Musa, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; nami nitaandika juu ya mbao hizo maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, hizo ulizozivunja.
2 Nawe uwe tayari asubuhi, na asubuhi ukwee juu katika mlima wa Sinai, nawe hudhurisha nafsi yako kwangu huko katika kilele cha mlima.
3 Asikwee mtu pamoja nawe, wala asionekane mtu awaye yote katika huo mlima; wala kondoo na ng’ombe wasilishe mbele ya huo mlima.
4 Naye akachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; na Musa akainuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama BWANA alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake.
5 BWANA akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA.
6 BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;
7 mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.