1 Na zile nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, wakafanya mavazi yaliyofumwa kwa ustadi sana kwa ajili ya kutumika katika mahali patakatifu, na kuyafanya hayo mavazi matakatifu ya Haruni, vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
2 Naye akaifanya hiyo naivera, ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa.
3 Nao wakaifua hiyo dhahabu hata ikawa mabamba membamba sana, kisha wakaikata iwe nyuzi, ili wapate kuifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyuzi nyekundu na za kitani nzuri, kazi ya fundi stadi sana.
4 Nao wakafanya na vipande vya mabegani kwa ajili yake, vilivyoungwa pamoja; viliungwa pamoja kwa ncha zake mbili.
5 Na huo mshipi wa kazi ya werevu, uliokuwa juu yake ili kuifunga mahali pake; ulikuwa wa kitu kimoja, na wa kazi moja na naivera ya dhahabu, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.