18 Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele.
19 Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.
20 Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
21 Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
22 Naye akafanya hiyo joho ya naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawi yote;
23 na hilo tundu lililokuwa katikati yake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, na utepe wake kulizunguka hilo tundu, ili lisipasuke.
24 Nao wakatia katika upindo wa joho makomamanga ya nyuzi za rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na rangi nyekundu, na kitani iliyosokotwa.