27 Nao wakafanya hizo kanzu za nguo ya kitani nzuri ya kufumwa, kwa Haruni, na kwa wanawe
28 na hicho kilemba cha nguo ya kitani nzuri, na zile kofia nzuri za kitani, na hizo suruali za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa,
29 na huo mshipi wa nguo nzuri ya kitani iliyosokotwa, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, kazi ya fundi mwenye kutia taraza; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
30 Nao wakafanya hilo bamba la hiyo taji takatifu la dhahabu safi, na kuandika juu yake andiko, mfano wa kuchorwa kwa muhuri, MTAKATIFU KWA BWANA.
31 Nao wakatia ukanda wa rangi ya samawi ili kulifunga katika hicho kilemba upande wa juu; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
32 Basi ndivyo ilivyomalizwa kazi yote ya maskani ya hema ya kukutania; na wana wa Israeli walifanya kama yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.
33 Nao wakamletea Musa hiyo maskani; yaani Hema, na vyombo vyake vyote, vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake;