15 Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaenda, wakamlilia Farao, wakisema, Mbona umetutendea hivi, sisi watumwa wako?
16 Watumwa wako hawapewi majani, nao wanatuambia, Fanyeni matofali; na tazama, watumwa wako wapigwa; lakini kosa hilo ni la watu wako mwenyewe.
17 Akasema, Wavivu ninyi; wavivu; kwa ajili hii mwasema, Tupe ruhusa twende kumtolea BWANA dhabihu.
18 Basi, enendeni sasa, mkafanye kazi; kwa maana hamtapewa majani, na pamoja na hayo mtaleta hesabu ile ile ya matofali.
19 Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wa katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza hesabu ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku.
20 Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wanasimama njiani, hapo walipotoka kwa Farao;
21 wakawaambia, BWANA awaangalie na kuamua; kwa kuwa mmefanya harufu yetu kuwa chukizo mbele ya Farao, na mbele ya watumishi wake, mkatia upanga mikononi mwao, watuue.