12 Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.
13 Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
14 BWANA akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao.
15 Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako.
16 Nawe umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa.
17 BWANA asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi BWANA; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu.
18 Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni.