1 BWANA akamwambia Musa, Ingia kwa Farao, ukamwambie, BWANA asema hivi, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia.
2 Tena kama ukikataa kuwapa ruhusa, tazama, nitaipiga mipaka yako yote kwa kuleta vyura;
3 na huo mto utafurika vyura, nao watakwea juu na kuingia ndani ya nyumba yako, na ndani ya chumba chako cha kulala, na juu ya kitanda chako, na ndani ya nyumba ya watumishi wako, na juu ya watu wako, na ndani ya meko yako, na ndani ya vyombo vyako vya kukandia unga.
4 Kisha hao vyura watakwea juu yako wewe, na juu ya watu wako, na juu ya watumishi wako wote.
5 BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha mkono wako na fimbo yako juu ya mito, juu ya vijito, na juu ya maziwa ya maji, ukawalete vyura waje juu ya nchi yote ya Misri.
6 Basi Haruni akaunyosha mkono wake juu ya maji yote ya Misri; na hao vyura wakakwea juu, wakaifunika nchi ya Misri.
7 Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri.