4 Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza.
5 Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja.
6 Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.
7 Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.
8 Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.
9 Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo.
10 Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.