1 Basi Yakobo akaona ya kuwa kuna nafaka katika Misri, Yakobo akawaambia wanawe, Kwa nini mnatazamana?
2 Akasema, Angalia, nimesikia ya kuwa kuna nafaka Misri; shukeni huko mkatununulie chakula, tupate kuishi wala tusife.
3 Basi ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri ili wanunue nafaka.
4 Walakini Benyamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumpeleka pamoja na ndugu zake, maana alisema, Mabaya yasimpate.
5 Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani.
6 Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake.
7 Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema. Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula.
8 Yusufu akawatambua nduguze, bali wao hawakumtambua yeye.
9 Yusufu akazikumbuka zile ndoto alizowaotea. Akawaambia, Wapelelezi ninyi, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.
10 Wakamwambia, Hasha, bwana, watumwa wako tumekuja ili tununue chakula.
11 Sisi sote ni wana wa mtu mmoja tu watu wa kweli sisi; watumwa wako si wapelelezi.
12 Akawaambia, Sivyo, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.
13 Wakamwambia, Sisi watumwa wako tu ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo, na mmoja hayuko.
14 Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi.
15 Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo.
16 Mpelekeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa, hata maneno yenu yahakikishwe, kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao, ninyi ni wapelelezi.
17 Akawatia wote gerezani siku tatu.
18 Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu.
19 Kama ni wa kweli ninyi ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu,
20 mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya.
21 Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata.
22 Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena.
23 Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao.
24 Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.
25 Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani.
26 Navyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakaweka nafaka yao juu ya punda zao, wakatoka huko.
27 Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake.
28 Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, N’nini hii Mungu aliyotutendea?
29 Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema,
30 Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi.
31 Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi.
32 Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani.
33 Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu.
34 Mkaniletee ndugu yenu mdogo; ndipo nitakapojua kama ninyi si wapelelezi, bali ni watu wa kweli; basi nitawarudishia ndugu yenu, nanyi mtafanya biashara katika nchi hii.
35 Ikawa walipomimina magunia yao, kumbe! Bahasha ya fedha ya kila mtu imo katika gunia lake. Nao walipoziona bahasha za fedha zao, wao na baba yao waliogopa.
36 Yakobo baba yao akawaambia, Mmeniondolea watoto wangu; Yusufu hayuko, wala Simeoni hayuko, na Benyamini mnataka kumchukua naye; mambo hayo yote yamenipata mimi.
37 Reubeni akamwambia babaye, akasema, Uwaue wanangu wawili nisipomrudisha kwako; mtie katika mikono yangu, nami nitamrudisha kwako.
38 Akasema, Mwanangu hatashuka pamoja nanyi, maana nduguye amekufa, naye amesalia peke yake; mabaya yakimpata katika njia mtakayoiendea ndipo mtakaposhusha mvi zangu kwa sikitiko mpaka kaburini.