1 Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote.
2 Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.
3 BWANA akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.
4 Yakobo akatuma watu, akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia,
5 Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.
6 Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu.
7 Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru.
8 Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia.
9 Hivi Mungu akamnyang’anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.
10 Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka.
11 Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa.
12 Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani.
13 Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa.
14 Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je! Imetubakia sehemu au urithi katika nyumba ya baba yetu?
15 Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa?
16 Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang’anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi yo yote Mungu aliyokuambia, uyafanye.
17 Ndipo Yakobo akaondoka, akapandisha wanawe na wakeze juu ya ngamia.
18 Akachukua wanyama wake wote, na mali yake yote aliyokuwa ameyapata, na wanyama aliowapata katika Padan-aramu, ili afike kwa Isaka babaye katika nchi ya Kanaani.
19 Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye.
20 Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia.
21 Basi akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, akaelekeza uso wake kwenda mlima wa Gileadi.
22 Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia,
23 akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi.
24 Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.
25 Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi.
26 Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga.
27 Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi?
28 Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu.
29 Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.
30 Basi sasa, umetoka kwa sababu umetamani sana nyumba ya baba yako. Mbona basi umeiiba miungu yangu?
31 Yakobo akajibu, akamwambia Labani, Kwa sababu naliogopa, nikasema, Usije ukaninyang’anya binti zako kwa nguvu.
32 Awaye yote utakayemwona kuwa nayo miungu yako, yeye asiishi. Mbele ya ndugu zetu ukitambue kilicho chako kwangu, ukakichukue. Maana Yakobo hakujua ya kwamba Raheli ameiiba.
33 Labani akaingia katika hema ya Yakobo, na hema ya Lea, na hema ya vijakazi wawili, wala hakuiona. Akatoka katika hema ya Lea, akaingia katika hema ya Raheli.
34 Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka katika matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala hakuviona.
35 Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala hakuviona vile vinyago.
36 Yakobo akakasirika, akagombana na Labani. Yakobo akajibu, akamwambia Labani, N’nini hatia yangu? Nayo ni nini dhambi yangu, hata ukanifuatia namna hii?
37 Umepapasa-papasa vyombo vyangu vyote; ni kitu gani ulichokiona cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu, na ndugu zako, wakaamue kati yetu.
38 Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala mbuzi zako wake hawakuharibu mimba wala waume katika wanyama wako sikuwala.
39 Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa kilichukuliwa usiku.
40 Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu.
41 Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara kumi.
42 Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa ungalinifukuza mikono mitupu. Mateso yangu na kazi za mikono yangu Mungu ameziona, akakukemea usiku huu.
43 Labani akajibu, akamwambia Yakobo, Hao binti ni binti zangu, na wana ni wanangu, na wanyama ni wanyama wangu, na yote uyaonayo ni yangu; nami naweza kuwatendea nini leo binti zangu na wana wao waliowalea?
44 Haya! Na tufanye agano, mimi na wewe, liwe kwa ushahidi kati ya mimi na wewe.
45 Yakobo akatwaa jiwe akalisimamisha kama nguzo.
46 Yakobo akawaambia ndugu zake, Kusanyeni mawe. Wakatwaa mawe, wakafanya chungu, nao wakala huko karibu na ile chungu.
47 Labani aliiita Yegarsahadutha, lakini Yakobo aliiita Galedi.
48 Labani akasema, Chungu hii ni shahidi kati ya mimi na wewe hivi leo. Kwa hiyo likaitwa jina lake Galedi,
49 na Mispa, maana alisema, Mungu avizie kati ya mimi na wewe, wakati tusipoonana.
50 Ukiwatesa binti zangu, na ukitwaa wake zaidi ya binti zangu, wala hapana mtu pamoja nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati ya mimi na wewe.
51 Labani akamwambia Yakobo, Tazama chungu hii utazame na nguzo niliyoitia kati ya mimi na wewe.
52 Chungu hii na iwe shahidi, na nguzo hii na iwe shahidi, ya kuwa mimi sitapita chungu hii kuja kwako, wala wewe hutapita chungu hii na nguzo hii uje kwangu, kwa madhara.
53 Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba yao, ahukumu kati yetu.Yakobo akaapa kwa Hofu ya Isaka baba yake.
54 Yakobo akachinja sadaka katika mlima, akawaita ndugu zake waje wale chakula, nao wakala chakula, wakakaa usiku kucha mlimani.
55 Labani akaondoka asubuhi na mapema, akawabusu wanawe na binti zake, akawabariki; kisha Labani akaenda zake, akarudi kwao.